Leo, September 7 2026 Mtandao wa watetezi wa haki za Binadamu
Tanzania (THRDC) imeshiriki katika Mkutano wa Kitaifa wa Wadau kuhusu Hali ya Siasa Tanzania ulioangazia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na Mwelekeo wa Baadaye, ulioandaliwa na Tanzania Centre for Democracy (TCD) jijini Dar es Salaam ambao Mgeni Rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais na waziri Mkuu mstaafu Mheshimiwa JAJI Joseph Sinde Warioba.
Mkutano huu wa siku mbili, umewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyombo vya habari, wasomi, watafiti, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, umetoa nafasi muhimu ya kutafakari hali ya kisiasa nchini, changamoto zilizotokea na nini kifanyike ili kutengeneza demokrasia iliyo ya kweli na ya wazii.
Kupitia ushiriki wake, THRDC inaendelea kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ya wazi na jumuishi, ushiriki wa wananchi katika masuala ya umma, kuheshimiwa kwa utawala wa sheria, ulinzi wa haki za binadamu na haki za kiraia na kisiasa, pamoja na kuimarisha imani ya wananchi katika taasisi za umma na michakato ya kidemokrasia.
Mazungumzo ya kitaifa yenye uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote ni msingi muhimu katika kujenga Tanzania yenye amani, umoja, demokrasia na utawala unaowajibika.